Mkuu wa Mkoa wa Manyara Azungumza na Watumishi wa Umma Wilayani Kiteto Leo Tarehe 05.07.2017
Imetumwa : July 5th, 2017
Mh. mkuu wa mkoa wa Manyara Dkt. Joel N. Bendera akizungumza na watumishi wa umma katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto.
Katibu tawala wa mkoa wa Manyara Bw. E. Maswi akizungumza na watumishi wa umma katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mh. T. Magessa akizungumza na watumishi wa umma katika mkutano huo.
Watumishi wa umma wakiwasikiliza kwa makini viongozi wao kama inavyoonekana katika picha.
Habari kamili.
Mh. mkuu wa mkoa wa Manyara Dkt. Joel N. Bendera amefanya ziara wilayani Kiteto kwa lengo la kuzungumza na watumishi wa umma. Katika ziara hiyo Mh. mkuu wa mkoa alifuatana na katibu tawala wa mkoa wa Manyara Bw. Eliakimu Maswi pamoja na maafisa waandamizi kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara.
Akizungumza na watumishi wa umma katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mh. mkuu wa mkoa wa Manyara amesema kwamba kila mtumishi wa umma anatakiwa kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yake. Uwajibikaji huo lazima uende sambamba na kufanya kazi kwa pamoja (team work) ambapo watumishi wote pamoja na wakuu wa idara wanatakiwa kufanya kazi kwa pamoja .Aidha mkuu wa mkoa amewataka wakuu wa idara kuwa na maono, uthubutu na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao, moyo wa uzalendo ni muhimu ili kuweza kusimamia kwa uangalifu,rasilimali zilizopo pamoja na mapato,na kuwa wabunifu na wenye bidii katika kutekeleza majukumu yao ili kutomkwamisha mkurugenzi wa halmashauri. Mkuu wa mkoa pia amewataka watumishi wa umma kubadili mitazamo yao, ili kuweza kuenda sambamba na kasi ya awamu ya tano.
Katika mkutano huo, katibu tawala wa mkoa wa Manyara amesisitiza uadilifu, ambapo watumishi wote wa umma wametakiwa kuwa waadilifu katika utumishi wao, kwani uadilifu ndio utakaowawezesha kuwatumikia vema wananchi kwa kuwapa huduma ambazo wananchi wataridhika na kwamba kwa kuwa waadilifu ndipo wataweza kujenga utumishi mzuri, usio na lawama kutoka kwa wananchi.
Naye mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amesema kwamba kila mtumishi abadilike ili kwenda na kasi ya awamu ya tano, kama kauli mbiu ilivyo ya hapa kazi tu, ni kufanya kazi kweli kweli.Lazima watumishi wote wa umma wakubali mabadiliko.
Pia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto bwana Tamim Kambona amesema kwamba uwezo wa halmashauri kimapato bado ni mdogo ukilinganisha na huduma ambazo halmashauri inatakiwa kuzitoa kwa wananchi na ukubwa wa eneo la wilaya ya Kiteto kijografia lakini watumishi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano, kuacha kuongea mambo ambayo hayana tija, na badala yake waongee yale ambayo yatasaidia kuwajenga zaidi ili kuboresha utendaji kazi katika halmashauri. Kadhalika Mkurugenzi amewataka wakuu wa idara kufanya kazi kwa bidii, na pale wanapokutana na changamoto yoyote wamshirikishe ili kwa kushirikiana nae waweze kutatua changamoto hizo.