Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza na Wakazi wa Kijiji cha Lembapuli kata ya Lorela Wilayani Kiteto
RC Mnyeti Atangaza Kiama kwa Wavamizi wa Misitu Kiteto.
Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexanda Mnyeti amewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kuvamia misitu na kukata miti kwa kisingizio cha mashamba.Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lembapuri kata ya Lorela wilayani Kiteto katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Lembapuri baada ya kuona uharibifu mkubwa alipotembelea msitu huo uliopo katika kijiji hicho kuona maeneo yanayotambulika na wananchi wa wilaya ya Kilindi na wilaya ya Kiteto kuwa ni mipaka kati ya wilaya hizo mbili kwa mujibu wa GN namba 65 ya mwaka 1961 na GN namba 185 ya mwaka 1980.
Akizungumza katika mkutano huo Mhe. Mnyeti amesema kwamba uharibifu wa misitu ni mkubwa sana, na inapaswa kuchukua hatua za haraka kukomesha uharibifu huo.Akisisitiza kuhusu kuchukuliwa hatua kali kwa wananchi wanaovamia misitu,Mhe. Mnyeti anasema ‘‘ mtu anapotaka kuvamia misitu chukueni hatua. OCD kamata watu wote waliovamia msitu wachukulie hatua za kisheria. Afisa misitu pitia maeneo yote yaliyovamiwa hesabu miti yote iliyokatwa ,wahusika wote wakisha malizana na polisi wapande miti .Na ukumbuke kwamba ni miti kumi kwa kila mti mmoja uliokatwa. Wapande miti hiyo chini ya uangalizi wa serikali”.
Katika hatua nyingine wakazi wa kijiji hicho wamewasilisha kero zao kwa mkuu wa mkoa ,ambapo kero kubwa ni wavamizi kutoka kijiji cha Mafisa Wilaya ya Kilindi, uvamizi ambao umedumu kwa miaka takribani kumi sasa, ambapo wavamizi hao wamekuwa wakisababisha uvunjifu wa Amani , Mauaji ,uharibifu wa mali,na uharibifu wa miundo mbinu ya maji .Kero nyingine ni kunyang’anywa mashamba yao yaliyopo katika kijiji cha Amei na kupewa watu wengine. Katika kushughulikia kero hiyo Mhe. Mnyeti Aliwataka wanakijiji hao hao kuwasilisha nyaraka zao halisi zinazoonyesha umiliki wa mashamba hayo kwa mkuu wa wilaya ili aweze kutatua mgogoro huo.Hapa Mhe. Mnyeti anasema “ Mkuu wa wilaya shughulikia tatizo hili la uvamizi wa Mashamba.Fukuza wote waliovamia mahamba ambayo sio ya kwao,waondoke maja moja.Ndani ya wiki moja wawe wameondoka ”.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Maggessa amemueleza Mhe. Mnyeti sababu ya kuendelea kwa mgogoro huo ambapo amesema kwamba watu wa Kilindi na Kiteto wanagombania mpaka, na kwamba watu wa Kilindi waliingia katika eneo linalosadikika kuwa ni eneo la Kiteto wakalifyeka wakatangaza kwamba ndio mpaka kati ya Kilindi na Kiteto jambo ambalo wananchi wa Kiteto hawakubaliani nalo. Vilevile Mhe. Magessa ametoa ushauri wa jinsi ya kumaliza mgogoro huo .Mhe. Magessa anasema ‘‘ Nashauri kwamba GN namba 185 ya mwaka 1980 ifutwe, na GN namba 65 ya mwaka 1961 ndiyo ifuatwe kuondoa huu utata uliopo sasa”.Akijibu kuhusu mgogoro huo wa Kilindi na Kiteto Mhe. Mnyeti amesema kwamba suala la mgogoro wa mipaka kati ya kilindi na Kiteto litashughulikiwa kikamilifu na litakwisha, na kwamba watakutana na waziri wa ardhi , viongozi wengine pamoja na wataalamu wa ardhi kujadili namna ya kumaliza mgogoro huo.
GN ni tangazo la serikali namba linaloainisha mipaka.Tangazo la serikali ndilo linaloeleza kwamba eneo fulani linaanzia wapi na kuishia wapi,iwe ni mkoa, wilaya ,tarafa, kata au kijiji. GN namba 185 ya mwaka 1980 na GN namba 65 ya mwaka 1961 ni matangazo ya serikali yanayoeleza mipaka kati ya Kilindi na Kiteto.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa