Naibu waziri wa Or -TAMISEMI Mhe. Mwita M. Waitara akitoa maelekezo kuhusu ujenzi wa jengo jipya la ofisi za halmashauri ya wilaya ya Kiteto , wakati wa ziara yake wilayani Kiteto mapema leo.
............. HABARI KAMILI ...........
Naibu waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mheshimiwa Mwita M. Waitara amesema kwamba kwa muda mfupi aliofanya ziara katika wilaya ya Kiteto ameona mambo mazuri ambayo anataka watu waje wajifunze .Mheshimiwa Waitara ameyasema hayo leo tarehe 15.12.2018 wakati wa ziara yake katika wilaya ya Kiteto , mkoani Manyara .
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi ya ujenzi katika shule za Sekondari za Kiteto na Engusero pamoja na shule ya msingi Twanga Mhe. Waitara amesema “Kwenye awamu hii kwenda mpaka Januari kuna fedha zitakuja, nimeona tayari zimeshatengwa kwa ajili ya ujenzi na madarasa na matundu ya vyoo kwa shule za msingi Kijungu,Makame na Mbikasi.Kwa mtindo ambao nimeuona hapa, naamini kwamba nyie Kiteto mtapata madarasa zaidi ya haya.Na ikiwezekana mzidishe usimamizi.Na sisi tutajitahidi tusukume ili fedha hizi zije , tuje tuangalie.Nitataka watu wafuate mtindo wenu, hii inaweza ikapunguza mzigo kwa serikali.Kwa sababu mahali pengine watu wanapewa 6,600,000/= wanajenga matundu sita ya vyoo wanakaa wanatulia, lakini nyie badala ya matundu sita mmejenga matundu 12 , badala ya madarasa matatu, mmejenga madarasa manne na ofisi na kwa fedha hizohizo mmetengeneza madawati 60.Ni lazima watu waje wajifunze kwa nini hapa imewezekana, na wao kwa nini wanashindwa’’.
Mheshimiwa Waitara amesema kwamba changamoto kubwa ambayo wao kama serikali wanayo ni matumizi ya fedha, na kwamba changamoto hiyo inatokana na watu kutumia fedha za serikali vibaya, watu kutojiongeza, ambapo wamekuwa wakiishia kutekeleza miradi kwa idadi ileile waliyopangiwa ,hata kama fedha hizo zingeweza kutosha kufanya zaidi ya idadi hiyo. Kitu ambacho kwa Kiteto imekuwa tofauti kwamba wamefuata maelekezo ya serikali, lakini pia wameweza kuongeza majengo na samani kwa kutumia kiasi hichohicho cha fedha, na zaidi ya yote wamezingatia viwango vya ubora katika ujenzi .
Mheshimiwa Waitara pia ameipongeza Halmashauri kwa kutumia fedha za ndani kwenye miradi mbalimbali, kama vile ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari ya Kiteto ,bweni ambalo limeshapauliwa, na ujenzi wa bwalo ,ambalo liko katika hatua ya lenta na kuongeza fedha kiasi cha shilingi 20,000,000/= katika umaliziaji wa mabweni na ununuzi wa vitanda katika shule ya sekondari ya Engusero pamoja na miradi mingine mingi katika sekta ya elimu na afya.Kadhalika mheshimiwa Waitara amewapongeza wakazi wa kiteto kwa uchangiaji mzuri wa miradi ya maendeleo sambamba na usimamizi mzuri wa miradi, jambo ambalo limewawezesha kutekeleza miradi mingi katika ubora. Aidha Mhe. Waziri amesema kwamba ameyapokea na ameahidi kuyafanyia kazi maombi yote yaliyowasilishwa wakati wa ziara yake .
Katika ziara yake hiyo ya siku moja Mhe Naibu waziri Waitara ametembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo.Maeneo hayo ni Jengo jipya la ofisi za halmashauri, shule ya msingi Twanga, Shule ya sekondari Engusero na shule ya sekondari ya Kiteto,ambako pamoja na ukaguzi wa ujenzi wa bweni ,pia ameweka jiwe la msingi katika bweni hilo.
..........MWISHO...........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa