Wakazi wa Kata ya Kijungu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti Katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kata ya Kijungu Wilayani Kiteto
................. HABARI KAMILI ..................
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Awataka Wanavijiji Kiteto Kuheshimu Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi.
Mkuu wa mkoa wa Manyara mheshimiwa Alexander Mnyeti amewataka wananchi wanaoishi vijijini kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi waliyojiwekea katika vijiji vyao. Mheshimiwa Mnyeti ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara ulifanyika katika kata ya Kijungu ,wilayani Kiteto kufuatia kero zilizowasilishwa na wananchi katika mkutano huo wa hadhara ambapo kero kubwa ni migogoro inayohusu wafugaji kuchungia kwenye mashamba ya wakulima na kuweka makazi kwenye maeneo ya mashamba,wakulima kuanzisha mashamba katika maeneo ya malisho,pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kutenga maeneo ya hifadhi bila utaratibu unaoeleweka na kusababisha baadhi ya wakulima kukosa maeneo ya kulima .
Akijibu kero hizo Mhe. Mnyeti amesema kwamba matumizi bora ya ardhi Katika vijijji yamepangwa na wanavijiji wenyewe,lakini wanavijiji hao hao ndio hawataki kufuata matumizi hayo. Mahali popote ambapo wananchi wameweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ,mipango hiyo iheshimiwe.Akitoa onyo kwa wanavijiji wanaotumia ardhi kinyume na mipango iliyowekwa Mhe. Mnyeti anasema “ Kuchungia kwenye mashamba ni kosa,kuvamia maeneo ya malisho na kutengeneza mashamba ni kosa, watu waishi kwa kuheshimiana.Mkulima amheshimu mfugaji ,na mfugaji amheshimu mkulima.Tatizo kubwa ninaloliona katika wilaya hii ni matumizi ya ardhi.Hili ni tatizo kubwa sana. Kama vijiji havikubaliani na mipango iliyopo sasa badilisheni. Mipango hiyo sio msahafu wala biblia , wanavijiji wakae wabadilishe matumizi . Hata hivyo Mheshimiwa Mnyeti amewataka wanavijiji hao kufuata utaratibu katika kufanya mabadiliko hayo ambapo anasema ‘‘ Mtu asibadilishe matumizi ya ardhi hadi vikao halali vikae vithibitishe mabadiliko hayo” Vilevile Mhe. Mnyeti amesema kwamba mabadiliko ya matumizi ya ardhi yatakapokuwa yamekubalika watu wasibadilishe ili kuepusha migogoro. Sambamba na hayo Mhe. Mnyeti ametoa miezi mitatu kwa mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa kushirikana na wataalamu wa ardhi wa halmashauri kukamilisha mchakato wa mabadiliko hayo.
Katika hatua nyingine Mhe. Mnyeti amewaagiza maafisa ugani kufanya tathimini stahiki kila inapotokea uharibifu wa mazao unaosababishwa na wafugaji kuchungia katika mashamba, na wasimamie wahusika wa mashamba hayo kulipwa mara moja .Pia amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kiteto SP Fadhili Luoga Kuwakamata wafugaji wote wanaofanya hivyo pamoja na ng’ombe zote zilizofanya uharibifu na kutoza faini kwa kila ng'ombe mmoja ili kukomesha vitendo hivyo.
Wilaya ya Kiteto imekuwa na migogoro ya ardhi ya muda mrefu ,migogoro ambayo inahusisha wakulima na wafugaji ,pamoja na kwamba kuna mipango ya matumizi bora ya ardhi ambayo imewekwa na vijiji vya wilaya hiyo ambapo mipango hiyo inaainisha maeneo ya kilimo, maeneo ya malisho na maeneo ya makazi.
................ MWISHO......................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa