Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe.Emmanuel Papian akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akitoa maelekezo ya serikali katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri .
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona akijibu hoja za Wahe. Madiwani katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri . Aliyekaa upande wake wa Kulia ni Mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Lairumbe Mollel na upande wake wa kushoto ni katibu wa CCM (W) ya Kiteto Ndg. Shekue Pashua.
Wahe. Madiwani wakiendelea na kikao cha baraza ndani ya ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto .
…………….HABARI KAMILI……………
Mbuge wa jimbo la Kiteto Mheshimiwa Emanuel Papian ametaka kuwepo kwa Takwimu sahihi za mifugo wilayani Kiteto ili kuokoa maisha ya wafugaji .Mheshimiwa Papian ameyasema hayo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto mwishoni mwa wiki.
Mheshimiwa Papiani amesema kwamba halmashauri inatakiwa kufanya jitihada za haraka katika kupata takwimu halisi za mifugo. Akisisitiza kuhusu umuhimu wa wilaya kuwa na takwimu sahihi za mifugo Mhe. Papian amesema “ Tutakapokuwa hatujapata takwimu halisi za mifugo,mtu ana ng’ombe 1000 ameandikiwa ng’ombe 500,serikali itakapokuja kukagua ikakuta ana mifugo 1000, ndipo udalali utakapo anza auction mart atasimama, ng’ombe zitapigwa mnada, wafugaji wetu watapata hasara”.
Vilevile Mhe Papiani amesema kwamba takwimu za mifugo ni muhimu sana katika kuwasaidia wafugaji kupata huduma stahiki za mifugo yao kutoka serikali kuu. Akisisitiza kuhusu umuhimu huo,Mhe Papian amesema “Kwa kupata takwimu sahihi za mifugo inatusaidia kupata namna ya kusukuma kupata hela kutoka serikali kuu za kuja kuchimba mabwawa na kufanya shughuli nyinginezo za mifugo.Kwa hiyo tunapotoa takwimu ndogo, hata serikali kuu inafanyia kazi hizo hizo takwimu ndogo.Kumbe maeneo yenye mifugo mingi ndiyo yalitakiwa yapewe kipaumbele katika kuchimbiwa mabwawa ,majosho na ukarabati wa vitu vingine”.
Aidha Mhe .Papian ametoa ushauri kwa Wahe. madiwani kwamba washirikiane na watendaji wa vijiji,wenyeviti wa vijiji na makatibu tarafa kuwaita wafugaji na kufanya nao hesabu ya idadi ya mifugo walio nayo na idadi ya mifugo iliyopigwa chapa,ili wapate idadi halisi, na idadi hiyo ipelekwe katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwa usalama wa wafugaji wanaoishi Kiteto.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel ameunga mkono ushauri wa Mhe. Papiani , ambapo amesema “Anachozungumza Mhe. mbunge ni kweli ,ni kwamba, hivi kama mtu akisema anataka kuchimba mabwawa Kiteto , atachimbaje kama hatuna takwimu halisi za mfugo? Ili tupate dawa za ruzuku,tupate mabwawa , na hata maeneo ya kulishia mifugo ni lazima tutoe takwimu halisi za mifugo iliyopo wilayani kwetu”.
Kikao hicho cha baraza la madiwani katika siku yake ya pili kimejadili ajenda tisa, ajenda ya tatu ikiwa ni kupokea maelekezo ya serikali ambapo mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa ametoa maelekezo juu ya masuala mbalimbali likiwemo suala la elimu,uandikishaji wa vitambulisho vya taifa , utaratibu wa uchomaji na uuzaji mkaa pamoja na upandaji miti.