Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akitoa maelekezo kuhusu namna ya kutekeleza zoezi la upandaji miti.Katika uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika katika eneo la mlima simu - kijiji cha Njoro, wilayani Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akipanda mti kama ishara ya kuzindua zoezi la upandaji miti .Tukio hili limefanyika katika eneo la mlima simu, kijiji cha Njoro wilayani Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akiunyweshea maji mti alioupanda ,katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti uliofanyika katika eneo la mlima simu, kijiji cha Njoro wilayani Kiteto.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akipanda mti katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti uliofanyika katika eneo la mlima simu, kijiji cha Njoro wilayani Kiteto.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona ( aliyevaa tisheti nyeupe yenye mistari ), waheshimiwa madiwani pamoja na watumishi wakiwa ndani ya basi lililowasafirisha kwenda katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti uliofanyika katika eneo la mlima simu- kijiji cha Njoro, wilayani Kiteto.
Watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto baada ya kumaliza kupanda miti katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti uliofanyika katika eneo la mlima simu, kijiji cha Njoro wilayani Kiteto.
Basi la Kampuni ya Struggle investment lililowasafirisha watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwenda katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti uliofanyika katika eneo la mlima simu - kijiji cha Njoro wilayani Kiteto.
..........HABARI KAMILI..........
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mheshimiwa Tumaini Magessa amewataka waheshimiwa madiwani kusimamia zoezi la upandaji miti katika kata zao.Mhe. Magessa ametoa agizo hilo baada ya kuzindua zoezi la upandaji miti ,uzinduzi ambao umefanyika katika eneo la mlima wenye minara ya simu maarufu kama mlima simu - kijiji cha Njoro , kata ya Njoro wilayani Kiteto mapema leo.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Mhe. Magessa amesema kwamba zoezi hilo la upandaji miti ni la kitaifa na kwamba kila wilaya inatakiwa kupanda miti isiyopungua 1,500,000.katika kuhakikisha kwamba zoezi hilo linatekelezwa Mhe. Magessa ametoa maelekezo ya namna ambavyo kazi hiyo itafanyika .Haya hapa ni maelekezo ya Mhe. Magessa ‘‘Tunatakiwa kupanda miche 1,500,000 katika wilaya yetu. Tumeitana hapa sio kwa sababu ya kuonyesha kwamba tunapanda nini leo,shida yetu kubwa ni kuanza kupanda miti leo.Katika eneo hili leo tutapanda miti 500,baada ya kumaliza hapa , zoezi hili linahamia kwenye kata. Tuna kata 23, kila kata itapanda miti 500. Kila diwani aliye hapa anakwenda kwenye kata yake kuhakikisha kwamba idadi ya miti aliyoambiwa kupanda anaipanda kwenye kata yake.Hili lifanyike kabla ya kuisha mwezi wa 4”.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel amesema kwamba zoezi hilo liwe endelevu kwa wananchi wa Kiteto,wapande miti kweye maeneo yao yote, maeneo ya taasisi pamoja na makazi yao ili kurudisha uoto wa asili.Akizungumzia madhara yaliyosababishwa na ukataji miti ovyo ambao ulikuwa ukifanyika siku za nyuma, Mhe Mollel amesema “tulifika mahali hali ilikuwa mbaya, hata mabadiliko ya tabia nchi yamesababishwa na ukataji miti.Lakini naamini wananchi wa Kiteto wamejifunza, wamejua madhara ya ukataji miti, na umuhimu wa kupanda miti.Wito wangu kwao ni kwamba tupande miti, tutunze mazingira ili tuweze kurudisha hali ya Kiteto kama ilivyokuwa zamani”.
Kadhalika mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamimu Kambona amesema kwamba zoezi hilo la upandaji miti ni la kitaifa,na wao kama halmashauri wamekwenda na watumishi katika uzinduzi wa zoezi hilo kwani watumishi ndio kioo cha jamii. Na kwamba watu wengi ambao sio watumishi wa serikali wanaangalia watumishi wanafanya nini ndipo na wao wafanye. Hivyo kitendo cha watumishi kushiriki katika uzinduzi huo kitawapa hamasa wananchi kujitokeza kwa wingi katika utekelezaji wa zoezi hilo. Aidha ndugu Kambona ameutaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) kulipa deni inalodaiwa na halmashauri ya wilaya ya Kiteto kiasi cha shilingi 42,000,000 (milioni arobaini na mbili) ili fedha hizo zitumike katika uendelezaji wa zoezi la kupanda miti wilayani Kiteto.
Zoezi hilo la upandaji miti litaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali wilayani Kiteto ndani ya mwezi April ,na linatarajiwa kurudiwa tena mwezi Julai 2018.