Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akigawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ,wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo uliuofanyika katika mji mdogo wa Kibaya,eneo maarufu kama chini ya mti.
Kamati ya ulinzi na usalama, Wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri pamoja na watumishi wakiwa katika uzinduzi wa zoezi la ugawaji vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania - wilaya ya Kiteto Ndg. Willjones Kisamba ( Aliyeshika kipaza sauti) akitoa ufafanuzi kuhusiana na wafanyabiashara wanaostahili kupewa kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo.
Wafanyabiashara wadogo wa Kiteto wakiwa wamekusanyika katika uzinduzi wa zoezi la ugawaji vitambulisho.
...............HABARI KAMILI.................
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe Tumaini Magessa amezindua zoezi la ugawaji vitambulisho vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daktari John Pombe Joseph Magufuli kwa wafanyabiashara wadogo.Uzinduzi huo umefanyika Kibaya mjini, eneo maarufu kama chini ya mti mwishoni mwa wiki.
Akizungumza kabla ya kuzindua zoezi hilo Mhe Magessa amewataka wafanyabiashara kuwa na leseni .Akisisitiza kuhusu hilo Mhe. Magessa amesema “Leseni ya biashara ni muhimu katika kuwatambua wafanyabiashara wanaolipa kodi.Siku nikipita kwenye biashara yako kuna moja kati ya haya mawili nataka niyaone; nione leseni ya biashara au kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo.Tunachotaka kusema ni hiki, tunategemea watu wote wanaofanya biashara tuwaone ama na kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo au leseni ya biashara.
Mheshimiwa Magessa ameendelea kusisitiza kuhusu wafanyabiashara kuwa na leseni ambapo amesema kwamba kuna watu wanafanya biashara,na wanastahili kulipa kodi TRA lakini hawana ‘tax clearrence’,au wanazo lakini wamezibana,hawakati leseni.Amesema kwamba ni lazima kila mfanyabiashara awe na leseni, kwani ndiyo inayomtambulisha kwamba ni mfanyabiashara halali . Amewataka wafanyabiashara kujijengea utamaduni wa kukata leseni na kulipa kodi.
Aidha Mhe. Magessa amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa iko nia njema ndani ya kiongozi wa nchi ambaye ni Mhe. Rais, ili kuonyesha muitikio chanya katika nia hiyo,wanapaswa kufanya biashara kwa bidii na kwa kufuata sheria ya kodi. Mheshimiwa Magessa amesema kwamba anaamini kuwa watu wa Kiteto ni wasikivu, hivyo watafanya kama sheria zinavyotaka.
Naye meneja wa TRA wilaya ya Kiteto ndugu Wiljones Kisamba ametoa ufafanuzi kuhusu wafanyabiashara ambao wanastahili kupewa kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo,ambapo amesema kwamba ni wale tu ambao mauzo yao kwa siku hayazidi shilingi 11,000, na kwa mwaka hayazidi shilingi 4,000,000/=. Amesisitiza kwamba wafanyabiashara ambao mauzo yao ni zaidi ya kiasi hicho cha pesa, hawastahili kupewa vitambulisho.
Kisamba pia amewataka wafanyabiashara kutowakimbia watumishi wa mamlaka ya mapato,badala yake wafike ofisini kwao ili wakae wazungumze nao, kufahamu kwamba ni kwa namna gani wanaweza kulipa kodi kwa utaratibu mzuri pasipo kuingia kwenye shida ya kufungiwa biashara.Amesema kwamba Mamlaka ya mapato sio adui wa mfanyabiashara, bali rafiki.
Kadhalika Kisamba amewakumbusha wafanyabiashara kufika katika semina ,pindi wanapotangaza kuwepo kwa semina ili waweze kuelewa mambo mbalimbali kuhusiana namna ya ulipaji kodi.Amesema kwamba wafanyabiashara wengi wamekuwa na tabia ya kutuma wafanyakazi wao kushiriki semina hizo, jambo ambalo ndilo linasababisha wao kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na tarattibu za ulipaji kodi.
Baada ya uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho Mhe. Magessa ameahidi kuwatembelea wafanyabiashara wote waliopewa vitambulisho hiyo kukagua biashara zao,ili kuhakikisha kwamba waliopewa vitambulisho hivyo wanastahili. Zoezi hilo litaendelea, ambapo wafanyabiashara ambao hawajapata vitambulisho hivyo wametakiwa kufika katika ofisi ya biashara ya halmashauri .
...............MWISHO....................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa