Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akizindua utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.Uzinduzi huo umefanyika katika hospitali ya wilaya.
Muuguzi akifanya matayarisho ili kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi ,katika uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika katika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Muuguzi akiwapa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi wanafunzi waliofika katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya kupata chanjo hiyo katika uzinduzi uliofanyika katika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Muuguzi akiwaelekeza wanafunzi kuhusu utaratibu wa kupata chanjo ya pili ya saratani ya mlango wa kizazi, baada ya kuwapa chanjo ya kwanza , katika uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akifuatilia kuhakikisha kwamba wanafunzi waliopewa chanjo, wameelewa vizuri kuhusu utaratibu wa kupata chanjo ya pili ya saratani ya mlango wa kizazi, katika uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Wanafunzi pamoja na mwalimu wao wakisubiri kupewa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi,wakati wa uzinduzi wa utoaji chanjo hiyo uliofanyika katika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
Viongozi wa dini, viongozi wa mila ,watendaji kata, pamoja wakazi mbalimbali wa wilaya ya Kiteto, wakiwa katika uzinduzi wa utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika hospitali ya wilaya ya Kiteto.
.......................HABARI KAMILI .................
Wilaya ya Kiteto imezindua chanjo ya saratani ya mlango wa Kizazi.Uzinduzi huo umefanywa leo na mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa katika hospitali ya wilaya .
Mhe. Tumaini Magessa amesema kwamba watoto wanahitaji kukingwa na saratani ya mlango wa kizazi, kwani jamii imekuwa ikiangamia kutokana na saratani hiyo.Akizungumza na wanafunzi wa kike waliofika kwa ajili ya kupata chanjo, Mhe. Magessa amewataka kutojiingiza katika kufanya mapenzi katika umri mdogo, Mhe. Magessa amesema “Mimba za utotoni ni tatizo kwenye hili,kuanza matendo ya watu wazima katika umri mdogo ni tatizo kwenye hili . Mtu asikudanganye ana bodaboda, kwamba mimi nitakuwa nakupeleka pale kaloleni shule ya msingi basi ukajua ni ofa, ukafika mahali ukajiingiza kwenye matendo ambayo ni ya watu wazima usikubali, ukikubali maana yake umejiingiza kwenye hatari ya kupata hili tatizo’’.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa wanafunzi hao kutokujihusisha na masuala ya kujamiiana,Mhe Magessa amesema “serikali imetoa kinga hii ,kuwa na kinga isiwe sababu ya kusema kwamba mimi sasa nimesha kingwa kwa hiyo sasa ni mwendo mdundo, utakutana na jingine tena mbele ya safari.Serikali imechukua jitihada hii ya kuwakinga,na ninyi mchukue jitihada ya kusema No. Kazi yenu ni rahisi sana,mjifunze kusema No.Sio kwa sababu serikali imewapa chajo,ndio mkimbilie kufanya matendo ya watu wazima”.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel amesema kwamba saratani ya mlango ya Kizazi imekuwa ni shida kwa kina mama,na kwamba ili kuidhibiti isiendelee kuwa sababu ya vifo kwa kina mama, ni vema wananchi wote wa wilaya ya Kiteto wenye watoto wa kike wa umri wa miaka 14 kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya ili kupata chanjo. Akisisitiza juu ya elimu ya saratani ya mlango wa kizazi na chanjo hiyo kuwafikia watu katika maeneo yote wilayani Kiteto, mhe. Mollel amesema ‘‘walimu,watendaji ,wakazi wa Kiteto pamoja na viongozi wetu wa mila nimewaona hapa.msambaze elimu hii vijijini na katika maeneo yote,ili watoto wote wa umri wa miaka 14 wapate chanjo hii.Ninawaomba sana ndugu zangu hii elimu itapakae kote.Ukiambiwa shida ya huu ugonjwa ni nini, unatamani hata mtoto wa mwaka mmoja achanjwe’’.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na kikao cha Huduma ya Afya ya Msingi ( PHC), ambapo ajenda kubwa ya kikao hicho ilikuwa ni ushirikishaji na utoaji hamasa juu ya utoaji chanjo ya saratani ya mlango ya kizazi kwa viongozi wa dini,viongozi wa mila pamoja na wazee maarufu , lengo likiwa ni kusaidia kuhamasisha jamii katika nyumba za ibada na maeneo wanayoishi. Katika kikao hicho Mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto Daktari Malkiadi Paschal Mbota ametoa elimu kuhusu saratani ya mlango wa kizazi ambapo amesema kwamba mimba za utotoni, kuanza kushiriki tendo la kujamiiana katika umri mdogo na kushiriki tendo la kujamiiana na wapenzi wengi ni miongoni mwa visababishi vya maambukizi ya virushi vya HPV ambavyo husababisha saratani ya mlango wa Kizazi. Aidha Dkt. Mbota amewataka wajumbe wa kikao hicho kuhamasisha jamii kupeleka watoto kupata chanjo ili kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo,sambamba na kuhuibiri jamii kubadili tabia na kuwa waaminifu katika mahusiano ya kimapenzi ili kuepuka maambukizi ya virusi vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi.
Mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto Dkt . Malkiadi Mbota akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa kufungua kikao cha Afya ya Msingi (PHC) kuhusu utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa halmashauri . Aliyekaa upande wake wa kulia ni kaimu katibu tawala wa wilaya Ndg. Fadhili Alexander.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akifungua kikao cha Huduma ya Afya ya Msingi (PHC) kuhusu utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa halmashauri .Aliyekaa upande wake wa kulia ni Mganga mkuu wa wilaya Dkt. Malkiadi Mbota, upande wake wa kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Ndg. Tamim Kambona.
Wajumbe wa kikao cha Huduma ya Afya ya Msingi (PHC) wakiendelea na kikao kuhusu utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa halmashauri .
..................... MWISHO.....................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa