Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kupitia mapato ya ndani kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 imetoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwaajili ya umaliziaji wa boma la zahanati iliyopo katika Kijiji cha Engusero Engine katika kata ya Chapakazi.
Machi 18, 2024, Mganga Mkuu wa Wilaya Dr. Vicent Gyunda kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, amefika katika eneo ambapo zahanati hiyo inajengwa na kuzungumza na viongozi wa chama na serikali, wajumbe wa kamati ya ujenzi na baadhi ya wananchi na kuwaeleza habari hiyo njema ya ukamilishaji wa zahanati hiyo.
Dr. Gyunda amesema kwamba pesa hiyo kwa kutamka ni nyingi ila kwenye utekelezaji ni ndogo hivyo amewaomba wananchi kuendelea kutoa nguvu kazi.
“Nitoe rai kwenu, kila mtu anapaswa awe jicho kwenye pesa hizi. Pia viongozi mnapaswa kuwahabarisha wanakijiji wengine wajue nini kinaendelea”, aliongeza Dr. Gyunda.
Nae mwenyekiti wa Kijiji hicho Ndg. Japhet Justani Kwanga, ameishukuru sana Halmashauri ya Wilaya kwa kutenga pesa hizo na ameahidi watatoa ushirikiano ili mradi upate kukamilika kwa wakati.
“Kwakweli tunashukuru sana na tumefurahi kuona serikali ya Mheshiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatujali” aliongeza Ndugu Kwanga.
Nae mmoja wa wananchi katika kijiji hicho, Ndg. Robert Abel Mpilimi ameshukuru ombi lao kusikilizwa na ameahidi kua wataunda kamati ya watu makini ili kuhakikisha mradi unakamilika vizuri na kwa wakati. “Sisi tumepewa fedha, kazi yetu sasa ni kutekeleza huu mradi ukamilike. Yaani wanasema Mungu akileta mvua haleti na wakulima ila sisi ndio wakulima hivyo serikali imeleta pesa kazi yetu sisi kukamlisha mradi”, aliongeza Ndg. Mpilimi.
Nae Mtendaji wa Kijiji hicho ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huo, Ndg Godwin Phabian Mbuya, amesema kwamba wanajiamini kwa nguvukazi, hivyo mradi utakamilika kwa wakati.
Wananchi wa kijiji hicho walianza na kukamilisha ujenzi wa boma hilo la zahanati mwaka 2020 baada ya kuwa wamekusanya michango ya ujenzi kwa muda wa miaka miwili. Mbali na nguvu kazi ya wananchi katika ujenzi wa boma hilo, pia limegharimu kiasi cha shilingi million 11.
Kukosekana kwa zahanati katika kijiji hicho kunawafanya wagonjwa na wajawazito wa kijijini hapo kwenda kupata huduma katika zahanati ya kijiji cha jirani, Osteti. Hali hii imekua adha kwao haswa katika kipindi cha masika ambapo daraja hufunikwa na maji na hivyo kuwafanya kushindwa kuvuka kwenda kupata matibabu. Umaliziwaji wa zanahati hiyo unatakiwa kukamilika ifikapo Juni 30,2024.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa