Halmashauri ya wilaya ya Kiteto imepania kuongeza ufaulu katika mitihani ya taifa kwa shule za msingi na sekondari mwaka 2017 wilayani Kiteto . Afisa elimu shule za msingi wilaya ya Kiteto bwana Emmanuel Mwagala amesema kwamba lengo la mkoa wa Manyara ni kufaulisha wanafunzi kwa asilimia themanini,na kwamba halmashauri ya wilaya ya kiteto chini ya Mkurugenzi wake makini bwana Tamim Kambona wamejipanga vema katika kuhakikisha kwamba lengo hilo linatimia kwa kuweka mikakati madhubuti ambapo idara ya elimu shule za msingi kwa kutumia maafisa elimu,waratibu elimu kata na walimu wakuu wa shule wanawajibika kufuatilia kwa karibu sana ufundishaji katika shule zote, kuhakikisha kwamba walimu wanawapa wanafunzi mazoezi ya mara kwa mara na mitihani mingi ya kujipima ili kuwaongezea uzoefu wa kujibu maswali ya mitihani ya taifa na kuwafanya wasome kwa bidii, pia walimu wakuu wa shule na waratibu elimu kata wameweka mkataba na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto wa kufikisha ufaulu wa asilimia themanini kwa kula kiapo cha kutimiza lengo hilo.
Aidha bwana Mwagala amesema kwamba tarehe 30/05/2017 hadi tarehe 01/06 /2017 wanafunzi wa darasa la saba mkoa wa Manyara walifanya mitihani ya utamilifu (Mock )ambapo kwa wilaya ya Kiteto matokeo yamekuwa mazuri sana yakilinganishwa na matokeo ya mwaka jana (2016), ambapo ufaulu ulishuka kidogo. Katika mitihani hiyo ya utamilifu 2017 wilaya ya Kiteto imeshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu wa jumla, katika shule kumi bora wilaya imetoa shule tano. Kwa upande wa wanafunzi kumi (10) bora wasichana, wilaya imetoa wanafunzi tisa (9) na kwa wanafunzi kumi (10) bora wavulana wilaya imetoa wanafunzi watano(5) . Nafasi hiyo ya ufaulu imekuwa faraja sana na kuongeza ari kwa Mkurugenzi wa halmashauri pamoja na idara ya elimu katika kuweka mikakati zaidi ili kufikisha na kuvuka lengo la ufaulu wa asilimia themanini. Shule zilizofanya vizuri katika mitihani hiyo ni Laalakir, Umoja, Boma, Sunya, Olchanyodo, Bwawani, Shekina,Nati, Lobosoiti na Azimio. Bwana Mwagala amesema kwamba shule ya msingi Laalakir imeendelea kufanya vizuri kwa miaka minne (4) mfululizo na kwamba wameweza kutunza nafasi yao ya ufaulu kwa kushika nafasi ya kwanza kwa miaka yote hiyo.
Kwa upande wa idara ya elimu Sekondari kaimu afisa elimu shule za sekondari wilaya ya Kiteto bwana Mtinga Maleya amesema kwamba wamejipanga kuongeza ufaulu kufikia lengo la mkoa la ufaulu wa asilimia themanini kwa kuweka mikakati ambayo ni kuhakikisha kwamba idara ya elimu sekondari wanafuatilia kwa karibu ufundishaji mashuleni. Kuhakikisha kwamba kuna mahudhurio mazuri darasani kwa walimu na wanafunzi, kuhakikisha kwamba walimu wanatoa mazoezi kila wiki na kila mwezi na mitihani ya utamilifu (Mock) inafanyika pamoja na kuhakikisha kwamba kunakuwa na upatikanaji samani(viti na meza) za kutosha ili wanafunzi waweze kukaa vizuri darasani wakati wanafundishwa. Aidha bwana Maleya amesema kwamba mikakati hiyo inatekelezwa kwa maafisa elimu kukaa na walimu kuangalia kazi wanazozifanya, ikiwemo ufundishaji, mazoezi na majaribio ya kila wiki na kila mwezi wanayotoa, kuangalia mafanikio na changamoto zinazowakabili katika ufundishaji na kuzifikisha katika mamlaka husika kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi, kufuatilia mahudhurio ya walimu na wanafunzi madarasani pamoja na kuangalia mgawanyo wa vipindi kwa walimu.
Aidha Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto ametoa mafuta kuhakikisha kwamba idara ya elimu wanafanya kazi ya kutembelea shule zote mara kwa mara kufuatilia na kuhimiza ufundishaji,utoaji wa mazoezi na mitihani mingi yakujipima ili kuiwezesha wilaya kupata matokeo mazuri zaidi katika mitihani ya taifa ya mwaka 2017. Pia mkurugenzi ametoa zawadi kwa shule za msingi na sekondari zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa mwaka 2016 kama motisha ya kufanya bidii ili kuendelea kupata ufaulu mzuri zaidi ambapo shule ya msingi Laalakir imezawadiwa shilingi milioni moja, shule ya msingi Boma imezawadiwa shilingi laki tano na Shule ya msingi Shekina imezawadiwa shilingi laki saba. Shule ya sekondari Kibaya imezawadiwa shilling milioni moja na shule ya sekondari Eko imezawadiwa shilingi laki saba. Kiasi hicho cha fedha kimetolewa kwa shule kulingana na vigezo vilivyotumika kikiwemo kigezo cha idadi ya wanafunzi katika shule hizo, na idadi ya wanafunzi ambayo shule hizo zimefaulisha.
Hata hivyo pamoja na jitihada zote hizo za kuongeza ufaulu idara ya elimu inakabiliwa na changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa 400, nyumba za walimu, ambapo walimu wanaishi mbali sana na shule wanakofundisha,na upungufu wa walimu 200.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa