Baraza la Madiwani Wilaya Kiteto limeridhia mabadiliko ya gharama za kumuona daktari katika Hospitali ya Wilaya kutoka TZS 12,000 hadi TZS 5,000.
Mabadiliko hayo yamepitishwa kwenye kikao cha Robo ya Kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Oktoba 22,2024 katika Ukumbi wa Maktaba ya Wilaya.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mabadiliko hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri (W) Kiteto, Mhe. Abdallah Bundala amesema kwamba wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto walikua wanatoa TZS 12,000 ikiwa ni ada ya kumuona daktari na bado walikua wanaendelea kulipia gharama za huduma nyingine kama vile vipimo na dawa.
Baada ya Baraza hilo kupitisha mabadiliko hayo, kuanzia Oktoba 22,2024 wagonjwa wanaoenda kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya Kiteto, watakua wanalipa TZS 5,000 ikiwa ni ada ya kumuona daktari ila wataendelea kulipia gharama nyingine kama vile vipimo na matibabu.
Mhe. Bundala aliendelea kueleza kua ada ya kumuona daktari katika zahanati na vituo vya afya itaendelea kubaki TZS 7,000.
“Tofauti ni kuwa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya walikua wanalipa TZS 12,000 kumuona daktari na kulipia huduma nyingine kama vile vipimo na dawa wakati wagonjwa katika zahanati na vituo vya afya wanalipa 7,000 gharama hiyo inajumuisha kumuona daktari pamoja na huduma nyingine kama vipimo na dawa. Hivyo gharama kwenye zahanati na vituo vya afya kwasasa itaendelea kuwa hiyohiyo 7,000 na inajumuisha huduma ikiwemo kumuona daktari, vipimo na dawa” amefafanua Mhe. Bundala.
Mabadiliko hayo ya bei yanakuja baada ya maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, ambaye alifanya ziara wilayani hapa mapema mwezi huu na kuagiza viongozi wa wilaya kukaa na kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo ili kumuwezesha mwananchi kupata huduma za afya hospitalini hapo kwa bei nafuu.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa